Saturday, February 25, 2012
VIRUSI HATARI ZAIDI YA UKIMWI
WANASAYANSI nchini Uholanzi wametengenezea virusi vinavyotishia kuua nusu ya watu duniani kote, vinavyoelezwa kuwa ni hatari zaidi ya vile vya Ukimwi.
Kwa mujibu wa habari zilizoenea duniani kote hivi karibuni zilizofichuliwa na Gazeti la Corriere della Sera la nchini Italia, Kituo cha Tiba cha Erasmus cha Uholanzi ndicho kilichohusika na utengenezaji wa virusi hivyo vya kuambukiza vinavyoweza kuua kwa kasi ya ajabu.
Gazeti hilo liliandika kuwa, utengenezaji huo uliokamilika mwishoni mwa mwaka jana uligundua kuwa virusi hivyo ni aina ya virusi vya mafua ya ndege vya H5N1 na kwamba vina uwezo wa kuambukizwa kwa njia ya hewa kwa mamilioni ya watu.
Mtaalamu wa Kituo cha Tiba cha Erasmus cha Uholanzi, Ron Fouchier alisema kuwa kirusi hicho kimepatikana kwa kufanya mabadiliko katika kirusi cha H5N1 (kile cha mafua ya ndege).
Ron aliongeza kuwa virusi hivyo ambavyo ni aina ya bakteria wanaohifadhiwa kwenye chupa ni miongoni mwa virusi hatari zaidi ambavyo vimekwishatengenezwa hadi sasa.
Utengenezaji wa virusi hivyo umezusha wasiwasi mkubwa huku wataalamu wakihoji hekima na sababu ya kupoteza mamilioni ya fedha kwa ajili ya ishu hiyo ambapo makundi ya kigaidi kama Al-Qaeda, Al-Shabaab na Boko Haram yakiinasa, yatamaliza watu duniani.