Tuesday, January 17, 2012

MTOTO WA LYUMBA AKAMATWANA MADAWA YA BILIONI 9.4


Watuhumiwa waliokamatwa na madawa hayo,wakwanza mwanamke ndio mtoto wa Lyumba ambae ni Morine wakiwa chini ya ulinzi.                                    
BAADHI ya wanasheria wamesema  watu wanne akiwemo Morine Amatus (22), anayetajwa kuwa ni mtoto wa Amatus Liyumba, waliokamatwa na  Jeshi  la Polisi mkoani Lindi wakishirikiana na Askari wa Kikosi cha Kupambana na Kuzuia Madawa ya Kulevya kutoka jijini Dar es Salaam, wakipatikana na hatia wanaweza kuhukumiwa kifungo cha maisha.
Watuhumiwa hao walikamatwa wakiwa na jumla ya kilo 210 za madawa aina ya Heroine, yenye thamani ya shilingi Bilioni 9.4.
Kamanda wa Kikosi cha Kuzuia na Kupambana na Madawa ya Kulevya Tanzania, Kamishna Mwandamizi Msaidizi wa Polisi, Godfrey Nzowa ambaye pia ni mwanasheria, aliliambia gazeti hili mwishoni mwa wiki iliyopita ofisini kwake kuwa iwapo watu hao watapatikana na hatia, hukumu yao itakuwa ni kifungo cha maisha jela.
“Miaka ya hivi karibuni huko Mtwara kuna watu walipatikana na madawa ya kulevya na kuhukumiwa kifungo cha maisha ambacho wanakitumikia,” alisema Kamanda Nzowa.
Mkuu huyo alifafanua kuwa kutokana na wingi wa madawa waliyokamatwa nayo, kesi hiyo itabidi isikilizwe na Mahakama Kuu ya Tanzania. 
“Upelelezi ukikamilika tutawafikisha mahakamani. Japokuwa tutawapeleka Mahakama ya Hakimu Mkazi Lindi, pale kesi yao itatajwa tu, lakini itakapoanza kusikilizwa itakuwa mahakama kuu,” alibainisha Nzowa.

WANASHERIA WANASEMAJE?
Matamshi hayo yaliungwa mkono na wakili maarufu nchini, Mabere Marando na Mwanasheria, Dk. Ngali Maita ambao kwa nyakati tofauti walisema adhabu ya kukutwa na madawa ya kulevya mengi kiasi hicho, huwa ni kifungo cha maisha.
“Unajua hukumu za kukutwa na madawa ya kulevya hutegemea, mara nyingi huwa ni kifungo cha miaka mingi, kuanzia miaka 20, 30 au maisha,” alisema Marando huku mwenzake, Dk. Ngali akiongeza kuwa anayepatikana na kilo 210 anahukumiwa kifungo cha maisha.
Watuhumiwa wengine waliokamatwa pamoja na Morine katika Kijiji cha Mchinga Mbili, Lindi kwa mujibu wa Nzowa ni mwenye nyumba yalipokutwa madawa hayo, Pendo Mohamed Cheusi (67), mkazi na mkulima wa kijiji hicho na Hemedi Said (27), dereva na mkazi wa Mtoni, jijini Dar es Salaam ambaye pia ni mtoto wa mwenye nyumba hiyo.
Aliwataja watuhumiwa wengine kuwa ni  Ismaili Adamu, kwa jina lingine Athuman Mohamed Nyaubi (28), mfanyabiashara wa magari nchini Afrika Kusini na mkazi wa Moroco jijini Dar es Salaam. 
Morine Amatus ni mkazi wa Mikocheni ‘B’ jijini Dar es Salaam na baba yake alikuwa Mkurugenzi wa Utumishi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT). Baba yake huyo alifungwa miaka miwili, Mei 24, 2010 kwa makosa ya kutumia vibaya ofisi ya umma.

 NZOWA KUDODOSWA
Alipododoswa zaidi Kamanda Nzowa, alisema kuwa wahalifu wengi wa madawa ya kulevya wanadhani sehemu salama ya kufanyia biashara hiyo haramu ni nje ya Dar es Salaam. 
“Niwatahadharishe wale wote wanaofanya au kufikiria kufanya biashara hiyo kwamba waache kwa sababu polisi kwa kushirikiana na raia wema tumejipanga. Maeneo yote siku hizi tunayalinda, watakaojiingiza katika biashara hiyo haramu, watakamatwa tu,” alionya Nzowa.
“Nitazungumzia day one tu (siku ya kwanza). Tuliwakamata usiku baada ya kuwazingira katika nyumba ya Bi. Pendo Cheusi. Tukawakuta na madawa yakiwa yamehifadhiwa ndani ya madumu yapatayo nane yaliyokuwa na ujazo wa lita 60 kila moja, tayari kusafirishwa kupelekwa nje ya nchi,” alisema.
Alibainisha kuwa tayari madawa hayo yamesafirishwa kuletwa jijini Dar es Salaam, ili yapelekwe kwa mkemia mkuu wa serikali kwa ajili ya kuyapima, sanjari na kuyatunza wakati kesi ya watuhumiwa hao itakapokuwa ikiendelea.
Kamanda Nzowa amewashukuru  wote waliofanikisha kutoa taarifa ya kuwepo kwa madawa hayo, na kuongeza kuwa hiyo ni mara ya kwanza kwa Mkoa wa Lindi kukamata madawa mengi kiasi hicho. 
Akawaomba wananchi kuendelea kushirikiana na vyombo vya dola kutoa taarifa pale wanapobaini kuwepo kwa vitendo ambavyo vinakwenda kinyume na maadili ya nchi.

UCHUNGUZI WETU
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umegundua kuwa watuhumiwa hao walikuwa wakifuatiliwa na polisi tangu walipokuwa wakitoka jijini Dar es Salaam, wakitumia boti iendayo kasi iliyokuwa ikipepea bendera ya nchi moja ya nje (jina tunalihifadhi).
Mwandishi wetu aliambiwa na baadhi ya wanakijiji wa Mchinga Mbili walioomba majina yao kutoandikwa gazetini, kuwa Hemedi alikuwa akifika kijijini hapo na rafiki zake mara kwa mara wakitumia magari tofauti ya kifahari.
Uchunguzi zaidi umebaini kuwa watuhumiwa hao walifikia hoteli moja ya kifahari ya mjini Lindi ambayo pango lake kwa siku moja ni shilingi 150,000 bila chakula na vinywaji. 
Habari za kipolisi zinasema mzee Amatus Liyumba, baba wa Morine naye atachunguzwa kutokana na mtoto wake kukumbwa na sakata hilo. Hata hivyo, hakuna kiongozi wa polisi aliyekuwa tayari kuthibitisha hilo kwa madai kuwa uchunguzi wao hufanywa kwa siri kubwa. 


Habari kwa hisani ya globalpublishers.