Thursday, March 22, 2012

BINADAM MWENZETU HUYU ANAOMBA MSAADA WETU JAMANI

MTOTO Honolata Juma Christian (8), (pichani) mkazi wa Mgeta wilayani Mvomero aliyetelekezwa na ndugu zake kutokana na maradhi ya ajabu yanayo msumbua, anataabika katika hospitali ya rufaa mjini hapa akiomba msaada wa shilingi 1,000,000 ili akatibiwe.
Gharama hizo ni za tiba,usafiri na matumizi katika Hospitali ya KCMC ya mjini Moshi ambako ameshauriwa kwenda na madaktari wa hospitali ya Mkoa wa Morogoro alikolazwa. 
Honolata ambaye tangu kuzaliwa kwake amekuwa akisumbuliwa na magonjwa likiwemo la kuota nywele mwili mzima, nundu mbili kichwani mithili ya pembe na matatizo ya macho.
Mtoto huyo analelewa na mama yake mzazi, Grace Francis (30) ambaye anadai ndugu zake wamemsusia na hawataki kumsaidia.
Akiwa hospitalini hapo wodi namba nne ,  Uwazi lilizungumza na mama huyo  ambaye alisema mtoto wake hivi sasa ameshindwa kuendelea na masomo kutokana na maradhi hayo ya ajabu.
 “Amefanyiwa uchunguzi na kugundulika kuwa jicho moja limekufa na asipopata tiba mapema la pili nalo litakufa, naomba msaada kwenu wasamaria,” alisema mama huyo huku akitokwa na machozi.
Akaongeza: “ Baada ya baba yake , Juma kufariki kwa kugongwa na gari shemeji,wifi na wakwe zangu wakamkataa wakisema sisi hatumtambui huyu mtoto mwache afe…nikaanza kuhangaika mahospitalini ikiwemo CCBRT ambako walimfanyia oparesheni ya jicho la kushoto ambalo anatumia kuonea,” alifafanua Grace. 
Walioguswa na habari hii wanaweza kumsaidia kwa kuwasiliana naye kwa namba ya simu 0713778024.