Mahakama nchini Ethiopia leo hii imewahukumu waandishi wa habari wawili wa Kisweden kifungo cha miaka 11 gerezani kutokana na tuhuma za kusaidia vitendo vya kigaidi na kuingia nchini humo kinyume cha sheria.
Hukumu hiyo imetolewa baada ya kukoselewa na makundi ya haki za binadamu. Jaji Shemsu Sirgaga aliiambia mahakama hiyo kwa lugha ya Amharic kwamba adahbu yao ni kutumikia kifungo cha miaka 11 jela.
Mwandishi Martin Schibbye na mpiga picha Johan Persson walikamatwa huko katika mkoa wa Ogaden Julai mosi, wakiongozana na waasi wa wa eneo hilo wa chama cha Ukombozi wa Ogaden, ONLF, baada ya kuingia Ethiopia kutokea Somalia.
Kufuatia hatua hiyo ya kuwatia hatiani waandishi hao wa habari, waziri mkuu wa Sweden, Fredrik Reinfeldt, amesema watuhumiwa hawana hatia na kutaka waachiwe huru.
Waasi wa ONLF wamekuwa wakipigania uhuru wao huko katika mkoa wa Ogaden kutoka kwa serikali ya Ethiopia tangu 1984, wakidai kwamba wanatengwa na utawala wa nchi hiyo.