Wednesday, December 14, 2011

MWANAMKE WA KISOUTH AFRICA AKAMATWA NA MADAWA THAILAND

 NOBANDA NOLUBABALO (23) kutoka Afrika Kusini jana alikamatwa akijaribu kusafirisha madawa ya kulevya aina ya cocaine katika nywele zake za rasta (dreadlocks) katika ndege iliyokuwa inakwenda Bangkok, nchini Thailand.

Nobanda  alikamatwa nchini Thailand na wanausalama waliohisi kulikuwa na kitu cheupe kwenye rasta zake ambapo walipomfanyia upekuzi wakagundua madawa hayo.

Uchunguzi uliofanyika baadaye uligundua kuwa dada huyo alipanda na madawa hayo kabla ya kupanda ndege iliyokuwa inatoka Brazil.

Madawa hayo yanakadiriwa kuwa na thamani ya  Pauni 93,000 ambazo ni sawa na sh. Milioni 235.3 ambapo yeye aliahidiwa kupewa Paundi 1,200 ambazo ni sawa na sh. Milioni tatu.

Kiasi cha kilo 1.5 kiligundulika kwenye rasta za dada huyo.

Nolubabalo bado anashikiliwa na vyombo vya usalama baada ya kukamatwa uwanja wa ndege wa Suvarnabhumi alipotoka katika ndege ya Shirika la Qatar ambayo ilikuwa imetokea Sao Paolo, Brazil, kupitia Doha.

Mwanamke huyo alisema kwamba alikubali kusafirisha madawa hayo baada ya kukubaliana na mfanyabiashara mmoja wa Thailand ambaye angempa Pauni 1,200.

Kukamatwa kwa raia huyo wa Afrika Kusini kunafuatia kunyongwa kwa raia mwingine wa nchi hiyo aliyekamatwa na madawa ya kulevya huko China.

Thailand hutoa adhabu kali dhidi ya wauza madawa ya kulevya ambapo ni pamoja na adhabu ya kifo.

Janice Linden (38) ambaye ni raia wa Afrika Kusini, aliuawa kwa kuchomwa sindano ya sumu jana baada ya kukamatwa katika jiji la Guangzhou, China,  na kilo tatu za madawa kama hayo Novemba 2008.