Tuesday, October 2, 2012

ANAHITAJI MSAADA WAKO MTOTO HUYU ILI APONE

NI mapenzi ya Mola! Hiyo ni kauli ya Bi. Veronica Laurent, mkazi wa Bunju  B Magengeni, Wilaya ya Kinondoni, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam, baada ya mwanaye, Godfrey Laurent (1) kuzaliwa huku mfumo wa sehemu ya kutolea haja kubwa ukiwa na hitilafu hivyo kuzuia uchafu kutoka. 
Akizungumza na Uwazi katika mahojiano maalum nyumbani kwake Bunju B mwishoni mwa wiki iliyopita, mama huyo alisema kuwa kufuatia tatizo hilo, mwanaye alipohitaji kujisaidia alikuwa akilia jambo lililomhuzunisha mzazi huyo na kuhitaji tiba ya tatizo hilo kwa haraka.
Alisema kuwa, kufuatia hali hiyo mbaya, alilazimika kumpeleka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambako baada ya kufanyiwa uchunguzi alifanyiwa upasuaji unaomuwezesha kujisaidia kupitia utumbo mpana.
“Madaktari walifikia uamuzi huo ili kuokoa maisha ya mwanangu yaliyokuwa hatarini kufuatia kuzaliwa bila kuwa na sehemu ya kutolea haja kubwa,” alisema kwa huzuni.
Aidha, aliongeza kuwa licha ya mwanaye  kufanyiwa upasuaji, anaishi katika mazingira magumu na hatarishi kufuatia utumbo kuwa nje.
Alisema kuwa kibaya zaidi, hana uwezo wala kupata msaada kutoka kwa mtu yeyote baada ya mwanaume aliyempa ujauzito kuingia mitini.
“Kwa hali hii sina ujanja, ninaishi na mwanangu kwa mateso makubwa  kama ambavyo unaona hali yake, haja kubwa inapitia tumboni,” mama huyo alimwambia mwandishi wetu huku akitiririkwa machozi.
Aliongeza kuwa, madaktari wamemwambia kama mwanaye atapelekwa kutibiwa nchini India atapona na kuishi maisha ya furaha kama watoto wengine.
‘“Naomba taasisi za dini, mashirika ya umma na Watanzania kwa jumla wanisaidie kupata shilingi milioni 10 zinazohitajika ili kuokoa maisha ya mwanangu,” alisema mama huyo.
Kwa yeyote aliyeguswa na mateso ya mtoto Godfrey awasiliane na mama yake kwa namba 0715 837 700  au atume fedha kupitia akaunti namba 10900159566 ya Benki ya Akiba Tawi la Tegeta Kibaoni, Dar.