KATIKA hali ya kuhuzunisha, Kigogo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM ) wa Kata ya Mafisi mkoani hapa, Bahati Pembe (43) amelazwa na familiya yake katika Hospitali ya Mkoa wa Morogoro, baada ya watu wasiojulikana kumvamia na kuilipua nyumba yake kwa petroli usiku wa manane wakiwa wamelala.
Tukio hilo la kuhuzunisha limetokea Alhamisi iliyopita Agosti 11 saa 7 usiku. Akisimulia mkasa huo kwa tabu kwenye wodi namba 4 hospitalini hapo, Bahati ambaye ni Katibu Mwenezi wa CCM Kata ya Mafisi alisema kwamba katika tukio hilo alijeruhiwa pamoja na watoto wake Anna Naloni (20), Zainabu Ally (14) Stella Hasala (7) na mjukuu wake Godfrey Sauti.
“Aliyeanza kugutuka ni mwanangu Zainabu ambapo alipiga kelele, tukaamka na kila mtu akawa anatafuta mlango wa kutoka akijaribu kunusuru roho yake, tulitoka ndani tukiwa na majeraha ya moto.
“Baada ya majirani kufika usiku huo na kufanya uchunguzi waligundua kuna watu waliimwagia mafuta ya petroli nyumba yetu kisha kuichoma moto na kutoweka bila kuiba kitu chochote,” alisema Bahati ambaye pia ni Diwani mstaafu wa Viti Maalumu wa kata hiyo.
Alipoulizwa kama tukio hilo analihusisha na mambo ya kisiasa, alikanusha na kuongeza kuwa huenda kuna watu wana chuki binafsi dhidi yake.
Vigogo wa CCM, Wilaya ya Morogoro mjini wakiongozwa na mwenyekiti wao wa wilaya, Fikiri Juma walimiminika hospitali kumjulia hali na polisi wamesema wanafanyia uchunguzi tukio hilo.
KWA HISANI YA GLOBAL PUBLISHERS.