Tuesday, August 23, 2011

MUNGU ACHEZEWI JAMANI NINI WAJIFUNZE WAFUASI WENU?

 MAMBO yameiva, Jumamosi iliyopita serikali ilitimiza ahadi ya kuwaonesha wabunge mkanda wa video wa mtandao haramu wa biashara ya madawa ya kulevya, ulio chini ya viongozi wa dini nchini.

Kufuatia mkanda huo, Uwazi lina habari kamili jinsi kikosi  kazi cha  kupambana na  madawa ya kulevya chini ya Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi,  Godfrey Nzowa, kilivyomnasa Askofu  Mkuu wa Kanisa la Lord Choose Charismatic Revived Church, Chidi Okechu.

 Okechu ambaye kanisa lake lipo Biafra, Kinondoni, Dar es Salaam ndiye anatajwa kuwa mkuu wa mtandao wa viongozi wa dini wauza madawa ya kulevya nchini.

ASKOFU NDEGE  TUNDUNI
Kwa mujibu wa Uchunguzi wa Uwazi, Machi 4, 2011 usiku wa manane, Kamanda Nzowa aliongoza kikosi chake na kuvamia nyumba aliyopanga askofu huyo, Kunduchi, Dar na kumkuta akiwa na kg 81 za heroine.

Askofu huyo alikamatwa akiwa na wapambe wake, Hycenth Stan, raia wa  Afrika Kusini, Shoaib Mohamed, Pakistan na Paul Ikechuwi Obi wa Nigeria, wote walikutwa kwenye nyumba hiyo yenye namba 593

KUNDUCHI NI PEPO YA WAUZA UNGA?
Uwazi limebaini kuwa mbali na askofu huyo na wapambe wake, msako mwingine wa Februari Pili, 2011, uliwezesha kunasa watuhumiwa wengine wa biashara ya madawa ya kulevya waliokutwa na kg 179, Kunduchi.

Waliokamatwa ni Fred William Chonde, mkazi  wa Mbezi Beach, Dar pamoja na raia wa Pakistan, Shahbaz Malik na Abdul Ghani ambao mbali na kukutwa na unga, pia walikutwa na shilingi milioni 15 kwenye gunia.
Habari zinasema, Februari 4, 2011, Abdallah Rajabu  alikamatwa Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere, Dar akiwa amemeza pipi 54 za cocaine, Juni Mosi, mwaka huu, Mwanaidi  Ramadhan Mfundo,  raia wa Kenya  na Watanzania Sara Daud Mnuo, Antony Athur Karanja  na Ben Nganer walikamatwa na kg 5 za cocaine na heroine.

Machi Pili, mwaka huu Chime Ajana alikamatwa Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere, Dar akiwa na kete 54 za cocaine, akijaribu kusafirisha kwenda Nigeria.
Habari zinasema kuwa watuhumiwa hao waliokamatwa ndiyo waliotoa siri nzito za viongozi wa dini wauza madawa ya kulevya, ikiwa ni pamoja na kuwezesha mtego uliomnasa Askofu Okechu.

MZEE WA KANISA NAYE MBARONI
Mzee wa kanisa moja ambalo halikutajwa, Raymond Gilbert Jungulu naye amekamatwa.

Wengine ambao wapo mahabusu wakituhumiwa kujihusisha na biashara ya madawa ya kulevya ni Bosi Chizenga, Ally Haji Mitanga, Gaban Abubakar na Gabar Diagar.

VIONGOZI WA DINI WAUZA UNGA NI WENGI
Kamanda Nzowa aliliambia Uwazi kuwa orodha ya wauza unga aliyopewa Rais Jakaya Kikwete  mwaka jana ipo na ina majina mengi ya viongozi wa dini.

Ripoti za kipolisi zinaliingiza matatani Kanisa Katoliki pamoja na Baraza Kuu la Waislam Tanzania (Bakwata), kwa maelezo kuwa kuna wauza unga ambao wamekuwa wakitumia mwamvuli wa taasisi hizo za dini.


Habari zinasema kuwa baadhi ya watu wasio waaminifu, huingia mpaka kwenye msafara wa Papa Benedict XVI na kupitisha unga kutoka sehemu moja kwenda nyingine kwa kuwa hawakaguliwi.


PENGO AIUDHI SERIKALI
Hatua ya serikali kuliambia bunge kwamba Kanisa Katoliki nalo ni mwamvuli wa biashara hiyo haramu, imekuja baada ya Askofu Mkuu wa kanisa hilo, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Kadinali Polycarp Pengo kuitibua ikulu.


Uchunguzi unaonesha, serikali ilichukizwa na kauli ya pengo kumwambia JK kwamba ni msaliti na hana ujasiri kama mwanamke mjamzito kwa sababu hajataja waziwazi majina ya watuhumiwa.


MAKANISA YA KIROHO YACHAFUKA
Gazeti hili limebaini kuwa tangu skendo ya viongozi wauza unga itajwe kwa mara ya kwanza na JK hivi karibuni, makanisa ya kiroho yamechafuka, huku viongozi wao wakituhumiwa moja kwa moja.

Pamoja na tuhuma hizo, Uwazi limebaini kuwa Askofu Zachary Kakobe, Mchungaji Getrude Rwakatare, Nabii Josephat Mwingira, Askofu Moses Kulola, Mchungaji Josephat Gwajima na wengineo ni wasafi, kwani bado hawajaingizwa kwenye skandali hiyo.

Baadhi ya maofisa  wa kikosi  kazi  waliongea  na mwandishi  wa habari  hii kwa sharti la kutotajwa majina yao walisema: “Nzowa yupo makini sana na kazi yake na angekuwa mtu mwenye tamaa ya fedha asingepata mafanikio.”

Nzowa alipozungumza na mwandishi wetu alisema: “Ninachoomba nipewe ushirikiano na wananchi kwa kuwa wao ndiyo askari wa kwanza.”

WABUNGE VILIO
Habari zinasema, baadhi ya wabunge walishindwa kuficha hisia zao na kutoa machozi walipokuwa wanaona mkanda wa video unaoonesha mtandao wa viongozi wauza unga.
Wabunge, walikwenda mbali zaidi na kushauri viongozi wote wa dini wauza unga wanyongwe.

Kwa hisani ya global publishers.