Wednesday, August 8, 2012

AAMUA KUJINYONGA BAADA YA KUTOA SIRI YA MAPOLISI WENZAKE


Askari polisi Kostebo Donald Mathew (Dunga) mwenye namba za kijeshi F3276 mkoani Morogoro ambaye aliibua tuhuma dhidi ya askari wenzake tisa kushirikiana na majambazi kupora na kubambikizia watu kesi, amekutwa amekufa huku mwili wake ukining’inia kwenye kamba juu ya mti.

Tukio hilo limetokea alfajiri jana ambapo mwili wa marehemu huyo ulikutwa katika mti uliopo kando ya daraja la mto Morogoro eneo eneo la Shani, baada ya kutambuliwa na baadhi ya wapita njia wakiwemo wauza magazeti.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Faustin Shilogile, alithibitisha kutokea kwa kifo hicho na kueleza kuwa taarifa za awali zinaonyesha kilitokana na kujinyonga bila kujua sababu ya kufanya hivyo.

Alisema kuwa marehemu alitumikia jeshi hilo kabla ya kuomba kuacha kazi mwishoni mwa mwaka jana na kwamba taratibu za kusafirisha mwili wa marehemu kupelekwa nyumbani kwao mkoa wa Kilimanjaro zinafanywa na jeshi hilo.

Siku moja kabla ya kukutwa na umauti, marehemu huyo alionekana eneo hilo akirandaranda kuanzia majira ya asubuhi mpaka usiku wa majira ya saa tano huku akionekana kama mtu aliyechanganyikiwa.

Baadhi ya mashuuda ambao hawakupenda kutaja majina yao, walieleza kuwa walimuona marehemu jana alfajiri katika eneo hilo akiwa ameshika kamba na kuizungusha na kisha baadaye kuona mwili wake pembezoni ya mti ukiwa unaning’nia.

Askari huyo aliyeajiriwa na Jeshi la Polisi karibu miaka zaidi ya 12 iliyopita, alijizolea umaarufu kutokana na kufichua uovu uliokuwa wakifanywa na wenzake katika kikosi cha kupambana na uharifu wa kutumia silaha (ant-robbery) hali hiyo ilipelekea kutoa taarifa kwenye vyombo mbalimbali vya habari baada ya kile alichodai viongozi wa juu wa jeshi hilo kufumbia macho madai hayo.

Baadhi ya  tuhuma hizo ambazo pia zilizochapishwa katika moja ya gazeti linalotoka mara mbili kwa  wiki mwaka jana, askari huyo alidaiwa kuwatuhumu askari hao tisa wa kikosi cha kupambana na majambazi wa kutumia silaha kupokea rushwa kutoka kwa wafanyabishara wa dawa za kulevya.

Tuhuma nyingine alizozitoa ni kuwa ni kukamata majambazi wa bunduki wakionyesha mali na fedha huwaachia na kuwaomba kuhamia mikoa mingine bila kuwafikisha kituoni, kupokea rushwa kutoka kwa wauza gongo, kusafirisha na kusindikiza bangi.

Tuhuma zingine zinazodaiwa kufanywa na askari hao ni kushirikiana na matapeli kutapeli raia na kushirikiana na wezi wa kuvunja na kuiba.

Hata hivyo, tuhuma hizo zilisababisha askari huyo, kukamatwa Novemba 11, mwaka jana kutokana na madai ya tuhuma hizo na kwamba Jeshi la Polisi makao makuu lililazimika kuunda kamati maalumu iliyochunguza madai ya askari waliohusishwa katika kashfa hiyo ambapo baadhi yao walihojiwa akiwemo marehemu.

Kukamilika kwa uchunguzi huo kulipelekea mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Said Mwema, kupangua kikosi  hicho mkoani Morogoro na baadhi ya askari kuhamishiwa vituo vingine vya kazi.